Mwandishi Mtanzania atunukiwa kushiriki program Muhimu ya Umoja wa Mataifa

Dar es Salaam Agosti 14, 2018-Mwandishi wa Habari kutoka Tanzania, Marygoreth Richard Makona, amechaguliwa na Umoja wa Mataifa kujiunga na program ya mafunzo yaani Fellowship ya Reham Al Farra kuanzia mwezi wa tisa hadi wa kumi mwaka huu katika makao makuu ya Umoja huo jijini New York nchini Marekani.

Programu ya Reham Al Farra ni fursa adhimu kwa waandishi wachanga kutoka nchi zinazoendelea na zenye uchumi unaolenga mabadiliko kushiriki katika kuifahamu zaidi na kuandika taarifa za Umoja wa Mataifa. Ni program inayolenga waandishi wachache inayofanyika kila mwezi wa tisa, sambamba na ufunguzi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Hivi sasa, mwandishi wa habari huyo anaifanyia kazi BBC Media Action kama mwandaaji mkuu wa kipindi cha Haba Na Haba kinacholenga zaidi vijana na kubadili mitizamo na tabia katika jamii. Kipindi hicho cha Haba na Haba hurushwa kupitia redio ya Radio Free Afrika kila Jumamosi asubuhi saa kumi na mbili na Jumapili saa kumi na mbili asubuhi katika idhaa ya Kiswahili ya BBC.

Alipoongea na kitengo cha habari cha Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam, Bi Marygoreth alisema, “kwangu hii fursa ni kitu kikubwa sana, kitanisaidia kwenda kujifunza zaidi juu ya kazi za Umoja wa Mataifa lakini pia kujua jinsi wanasimamia agenda mbalimbali. Na kwa sababu nitatembelea ofisi na maofisa mbalimbali wanaosimamia ajenda hizo nitaezielewa zaidi na kuelewa jinsi ya kufikisha uelewa ntakaoupata vizuri zaidi kwa wananchi wa kawaida.”

Awali kabla ya kupata fursa hii, Bi Marygoreth alifanyakazi na redio jamii, TV1, EATV ambapo alikuwa mtangazaji kwa miaka kadhaa. Alipata fursa hii baada ya kutuma maombi kupitia kwenye Mtandao.

Nchi zingine zilizofanikiwa kuwa na mwandishi mahiri ni pamoja na Uganda, Kenya, Burundi, Serbia, Bangladesh, India, Venezuela, Nigeria, Afghanistan, Sri Lanka, Trinidad and Tobago, Turkey, Nicaragua na Kuwait.

Inatarajiwa katika kipindi cha wiki tatu za mwezi wa tisa na wa kumi mwaka huu, Marygoreth pamoja na wenzake walionufaika na program hii, watashiriki katika kuandika taarifa za Baraza Kuu la 73 la Umoja wa Mataifa  pamoja na kufanya kazi za kuhoji maafisa wakuu wa UN kwa weledi.  Vile vile watashiriki mikutano mifupi ya kupata taarifa kutoka kwa maafisa wakuu wa idara na shirika mbalimbai za Umoja wa Mataifa na kubadilishana mawazo na watu kutoka nchi mbalimbali duniani.

Washiriki wa miaka ya nyuma waliwahi kukutana na Katibu Mkuu wa UN, Raisi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Wawakilishi wa Kudumu wa Nchi mbalimbali ndani ya Umoja wa Mataifa.  Programu hii pia huwatembeza waandishi waliotunukiwa kushiriki katika ofisi za habari zilizopo Marekani kama New York Times, Democracy Now! Na WNTC radio.

Kulingana na Bi Bayann Hamid, Afisa Habari msaidizi wa Kitengo cha Habari cha jijini New York(UNDPI), Marygoreth atakuwa mwandishi wa sita kushiriki mpango huu kutoka Tanzania waandishi watanzania   waliowahi kushiriki mpango huu ni pamoja na Assumpta Massoi aliyetunukiwa mwaka 2000 na ambaye hivi sasa anaifanyia kazi Redio ya Umoja wa Mataifa-UN Radio, Joseph Kithama alishiriki 1987, John Waluye -mwaka 1987, Zuhura Sunday Ernest  alishiriki 1986 na Mikidadi Mahmood mwaka 1981.

Kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa kinawakaribisha waandishi wa Habari kushiriki fursa mbalimbali za umoja wa Mataifa zinazotangazwa kwenye Mtandao wa Umoja huo.

Programu ya Reham Al Farra iliidhinishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia Azimio la 35/201 mwaka 1980.  Awali ilifahamika kama program ya Idara ya Habari ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watangazaji na waandishi kutoka nchi zinazoendelea. Programme hii ilipewa jina la Reham Al-Farra ambaye alikuwa Afisa Habari mwenye miaka 29 kutoka Jordan ambaye aliuawa katika shambulizi la bomu katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa nchini Baghdad tarehe 19 mwezi Agosti, 2003.

Tangu kuanzishwa kwa mpango huu wa uelimishaji mwaka 1981, Zaidi ya waandishi 581 kutoka nchi 168 wametunukiwa na kufaidika na program hii. Baada ya kukamilisha mafunzo hayo maalum, wahitimu hupaswa kuendelea kufanya kazi za uandishi wa habari na kuinua uelewa wa Umoja wa Mataifa katika nchi wanakotokea.  Programu hii haitoi mafunzo ya awali ya uandishi kwa kuwa wahitimu wanakuwa tayari wamesomea na wanafanyia kazi katika fani ya Uandishi wa Habari.

Fellowship hii itagharimikia nauli, malazi, chakula na safari nzima ya Bi Marygoreth pamoja na kumpa fedha za kujikimu kwa kila siku atakapokuwa jijini New York.

Imeandikwa na

Stella Vuzo, Afisa Habari

Kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa, Dar es Salaam

This entry was posted in Latest news on by .

About STELLA VUZO

UNIC Dar es Salaam is pleased to be of service to the people of Tanzania, providing prompt and accurate information on the work of the United Nations. Please share your views and comments. You can also engage our discussions on unicdaressalaam facebook page and follow us on twitter@UNICDaressalaam.