TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI-MAADHIMISHO YA NELSON MANDELA

“One way we can build a better future for children is by empowering them through allowing them to speak up for themselves.”-NELSON MANDELA

Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela itaadhimishwa na Ubalozi wa Afrika Kusini kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika shule ya Viziwi iliyopo Buguruni Malapa, jijini Dar es Salaam siku ya Jumatano tarehe 18 mwezi huu.

Maadhimisho haya yaliaasisiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia Azimio la Novemba 2009 lenye nambari; A/RES/64/13  lililopitisha Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kutokana na kazi zake za kuleta Amani na Uhuru.

Katika siku hii, watu duniani kote wanaalikwa kufanya kazi za kujitolea kwa muda wa dakika sitini na saba kwa kumuenzi Nelson Mandela ambaye iwapo angekuwa hai mwaka huu angekuwa anatimiza miaka mia moja. Kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ni, “Chukua hatua dhidi ya umasikini, ulete mabadiliko”

Siku hii ya kimataifa ya Nelson Mandela inasherehekea maisha na mema mengi aliyoyafanya Nelson Mandela enzi za uhai wake. Ni siku tunapokumbuka kujitolea kwake kutatua migogoro, kuboresha mahusiano ya watu wenye asili na rangi tofauti, kusamehe wengine, kuboresha haki za binadamu, kuendeleza usawa wa kijinsia, haki za watoto na wanyonge pamoja na kupambana dhidi ya umasikini na kujenga misingi ya haki kwenye jamii.

Inatarajiwa kwamba mabalozi na wawakilishi wao, wafanyakazi wa UN, Makampuni ya Afrika Kusini na wananchi wa Afrika kusini waliopo nchini, vijana, na wananchi wa kawaida watajumuika shuleni hapo ili kushiriki kujenga jiko, kufyeka majani, kusafisha madarasa, vyoo na ofisi za walimu vile vile inatarajiwa wanafunzi na walimu viziwi wataungana na wageni wao katika kubadilishana mawazo na kushiriki shughuli mbali mbali za kujitolea.

Waandishi wa habari mnaalikwa kuja kushiriki katika maadhimisho haya na pia kuchukua habari mbalimbali kutoka kwa watakaohudhuria.

Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, kutakuwa na mikutano isiyo rasmi kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa ambapo rais wa Baraza Kuu pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa watazungumza.  Kwa taarifa zaidi tembelea tovuti ifuatayo;

Kwa taarifa za mitandaoni kuna hashtag zifuatazo zinazotumika duniani kote.

Website: www.un.org/en/events/mandeladay/ . Hashtags: #MandelaDay , #Mandela100.

Shughuli itaanza saa tatu na kuisha saa tano asubuhi.

NANI:                    UBALOZI WA AFRIKA KUSINI NA UMOJA WA MATAIFA

NINI:                     MAADHIMISHO -SIKU YA KIMATAIFA YA NELSOM MANDELA

WAPI:                 SHULE YA BUGURUNI VIZIWI, MALAPA BARABARA YA UHURU

LINI:                     JUMATANO TAREHE 18, JULAI, 2018

LOCATION:         https://goo.gl/maps/6y3AQoD7SLN2