VIJANA WAPATA ELIMU KUHUSU MAUAJI YA MOTO YALIYOONGOZWA NA HITLER

Dar es Salaam, 26 January 2017-Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam-UNIC kwa kushirikiana na Ubalozi wa Ujerumani, Shule za Sekondari, vijana ambao hawapo shuleni na Asasi za kiraia leo hii wameadhimisha siku ya kimatiafa ya kumbukumbu ya wahanga wa mauaji ya moto (holocaust) katika ukumbi wa British Council jijini.

Kauli mbiu yaa Mwaka huu ni, “Kumbukumbu ya mauaji ya moto: kuelimisha jamii kwa maisha bora ya baadae.”
Siku hii imepangwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia Azimio 60/7 la Novemba 2005 linalohamasisha nchi wanachama wa Umoja huo kuelimisha jamii zake kuhusu Mauaji ya moto ili isije ikatokea tena duniani.

Mgeni rasmi alikuwa Bi Susan Keller, Afisa  wa Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania ambaye pia anahusika na habari za ubalozi huo nchini. Katika tamko lake alisema, “Kama Mjerumani, binafsi najisikia huruma,hasira na kujutia kuhusu huu uhalifu uliotendwa na watu wa Ujerumani. Hii ndiyo sababu nipo hapa, nikihitaji kujibu maswali na kuelimisha wote kwamba uwajibikaji haupo tu kwa wahenga wetu bali hata kwenye kizazi kinachofuatia.”

Bi Keller aliasa kwamba, “leo hii wote tunasikiliza redio na kuwafuata watu maarufu mitandaoni na kwenye Facebook na twitter.  Tunatuma ujumbe na video kabla hata ya kusoma na kuzitizama hadi mwisho, wakati mwingine hata hatufahamu iwapo taarifa ni ya kweli au la.  Watoto wananyanyaswa shuleni na wanawake kufanyiwa ukatili vijijini, miaka themanini imepita na leo hii tupo hapa, ni lazima tuwe makini na kile ambacho watu wengine wanataka tuamini.  Tupo hapa kwa ajili ya kujifunza, tusiruhusu wageni kutoka nje ya nchi au hata watu nchini mwetu kuteseka, kutoheshimiwa au kutuhumiwa visisivyo.”

Katika taarifa ya Katibu Mkuu Antonio Guterres iliyosomwa na Mkuu wa Kituo cha Habari cha UN, Stella Vuzo, Mkuu huyo wa Umoja wa mataifa ameongoza kwamba, “Dunia inawajibika kukumbuka ya kwamba mauaji ya moto yalikuwa ni mauaji yaliyopangwa ili kuwatokomeza wayahudi na watu wengine. Itakuwa makosa makubwa kudhani ya kwamba Mauaji ya moto ni matokeo ya uenda uwazimu wa kikundi cha wahalifu wa Nazi.  Kinyume na dhana hii, Mauaji ya moto yalijumuisha chuki, kutoana ‘sadaka’ hali ilipoenda mrama na ubaguzi uliowalenga wayahudi katika kile tunachokiita leo kuwa ubaguzi wa rangi na ukabila.

Katibu Mkuu anasikitishwa kwamba Dunia ya leo inazidi kukumbwa na hali ya watu kukithiri katika matendo ya ubaguzi wa rangi na kuendeleza chuki dhidi ya waislamu.  Hali ya kutokufikiri na kukosa uvumilivu imerudi.  Hali ambayo amesisitiza, “Hatupaswi kamwe kubaki kimya wakati binadamu wenzetu wanateseka, lazima tuwatetee wanyonge na kuwatia hatiani wanaokiuka misingi ya haki”

Vijana kutoka shule mbali mbali walipata fursa kuuliza maswali.  Kwa mfano mwanafunzi Martha Mushi kutoka Airwing Sekondari alimuuliza Afisa wa Ubalozi wa Ujerumani, Susann Keller iwapo kuna adhabu za aina yoyote zilizotolewa kwa walioshiriki mauaji chini ya utawala wa Adolf Hitler.  Bi Susann alimjibu kwamba kuna mahakama ya Nuremberg nchini Ujerumani ambayo inaendelea kuwakamata watuhumiwa na kusikiliza kesi zao.  Alisema watuhumiwa wengi wanakamatiwa Amerika ya Kusini.

Vijana kutoka Asasi za kiraia walitaka kufahamu hatima ya Adolf Hitler nao wakajibiwa kwamba Adolf Hitler alijipiga risasi na kujiua na kwamba wayahudi waliokuwepo kwenye kambi maalum za mauzji waliokolewa na majeshi kutoka nchi mbali mbali ikiwemo Marekani, Uingereza, Ufaransa na Warusi waliofika kambi la Birkenau nchini Poland na kuokoa wahanga waliobaki.

Wayahudi takriban milioni sita waliouwawa chini ya utawala wa Adolf Hitler nchini Ujerumani katika kipindi cha 1933-1945.

Shule zilizoshiriki ni Chang’ombe, Kibasila, Jitegemee, Kigamboni, Dar es sallam, Gerezani, Airwing na Temeke Youth Development Network na asasi za kiraia.

Jumla ya vijana mia moja walipata mafunzo hayo endelevu ambapo pia walitizama filamu kuhusu historia ya mauaji ya moto yaliyotendwa na chama cha Nazi likiongozwa na Chansela Adolf Hitler aliyeiongoza Ujerumani wakati huo na kutizama maonesho yaliyobandikwa ukutani yakiwa na mlolongo wa matukio kabla na baada ya utawala wa Dikteta Hitler, utawala ambao ulileta maafa ya mauaji ya moto.
Picha zote na Harriet Macha na Laurean Kiiza wa UNIC Dar es Salaam.

Tafadhali tembelea tovuti hii kwa taarifa zaidi: http://www.un.org/en/holocaustremembrance/