UN TANZANIA YAZINDUA MALENGO YA MAENDELEO ENDELEVU

Dar es Salaam, Tanzania, Septemba 29, 2015:
UMOJA wa Mataifa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, leo wamezindua rasmi malengo ya maendeleo endelevu 17 ( SDGs) katika hafla fupi iliyofanyika katika hoteli ya Serena,jijini Dar es Salaam na kuhuduhuriwa na mabalozi, maofisa wa UN na serikali, waandishi wa habari, mashirika yasiyo ya kiserikali na vijana.

Uzinduzi wa malengo hayo ambayo pia yanajulikana kama malengo ya dunia ulifanywa na Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania ambaye pia ni Mwakilishi Mkazi wa UNDP Bw. Alvaro Rodriguez, Kamishna Paul Kessy kutoka Tume ya Taifa ya Mipango (POPC), na kamishina Ahmed Makame Kutoka Tume ya Mipango ya Zanzibar, waliowakilisha serikali, Balozi Fionnuala Gilsenan wa Ireland na Bi. Liz Lloyd, Ofisa mtendaji mkuu wa Benki ya Standard Chartered kwa niaba ya wadau wa mradi wa Project Everyone Partners.

Malengo hayo 17 ni wito wa dunia wa kuchua hatua za kuufuta umaskini, kuihami dunia dhidi ya uharibifu wa mazingira na kuhakikisha kwamba kila mwanadamu anaishi maisha stahiki katika amani na ustawi.
Katika malengo hayo 17 yapo makusudio 169 yanayotoa ramani ya utengenezaji wa sera za maendeleo na namna ya kutekeleza kwa miaka 15 ijayo.
Malengo hayo yaliyojengwa juu ya mafanikio ya malengo ya milenia (MDGs) yanayofikia tamati desemba 2015, yameingiza vitu vipya kama mapambano dhidi ya tofauti za kiuchumi, ubunifu, mabadiliko ya tabia nchi,lishe, amani na haki. Malengo haya ni mpango wa dunia unaojikita kwa ustawi wa wananchi na dunia.
Akizungumza umuhimu wa malengo hayo, Bw. Rodriguez amesema: “Kwa mara ya kwanza katika historia ya dunia, serikali zimekutana na kukubaliana kupeana malengo kwa ajili ya kila mtu. Malengo haya yatasaidia mataifa yote kushirikiana katika kuwezesha ustawi, kupunguza matumizi na kuilinda dunia dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.Katika hilo watashughulikia voashiria vinavyohusu maendeleo endelevu: ukuaji wa uchumi, ustawi wa jamii na kulinda mazingira.”

Akizungumzia malengo hayo Bw. Kessy amesema kwamba serikali ya Tanzania ipo tayari kuyatekeleza malengo hayo kikamilifu ili kuleta maisha bora kwa watu wake.

Alisema kwamba Rais Jakaya Kikwete alikuwa jijini New York, Marekani kwa ajili ya kutia saini malengo hayo na huo ni uthibitisho wa namna serikali ya Tanzania ilivyo tayari kushirikiana na wadau wengine kuufuta umaskini.

Naye kamishna Makame alisema Zbar ilishirikishwa kikamilifu katika mchakato wa kukusanya maoni juu ya malengo hayo na watatumia uzoefu wlaioupata katika utekelezaji wa malengo ya milenia ili kuhakikisha utekelezaji wa malengo haya mapya unafanikiwa.

“Ninafurahi kusema kwamba Zanzibar tuko katika mchakato wa kutengeneza mkakati wa maendeleo wa kitaifa na malengo haya mapya yatajumuishwa kikamilifu katika mkakati huo,”alisema.

Akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kufanikisha maendeleo, Balozi Fionnuala amesema taifa lake Ireland lipo tayari kusaidia kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.

“Malengo ya dunia yaliyojengwa katika Malengo ya Milenia yamelenga kukabiliana na matatizo ya zamani kwa mbinu mpya. Yamelenga kukabiliana na tatizo la umaskini na ukosefu wa usawa katika masuala ya uchumi.SDGs haiwezi kufanikiwa bila kuyaangalia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, usawa wa jinsia, haki za biandamu na kukabiliana na mfumo unaobagua,” alisisitiza Balozi Fionnuala.

Akizungumza kwa niaba ya wadau wa Project Everyone, Bi Liz Lloyd alielezea umuhimu wa sekta binafsi kushirikiana na Umoja wa Mataifa na serikali ya Tanzania katika kusambaza elimu juu ya malengo haya ya dunia ili watu wa kada zote waweze kuayelewa kikamilifu na kushiriki katika utekelezaji wake.

“Malengo ya Dunia yanatoa nafasi adhimu ya ushirikiano na taasisi kubwa duniani, kutekeleza malengo 17 kwa nia ya kufufua ushirikiano wa dunia kwa maendeleo endelevu. Benki ya Standard Chartered inajisikia furaha ya kuwa nchini Tanzania kwa miaka mingi na inatumaini kwamba kwa ushirikiano huu kila mtu anayeishi nchini hapa atafaidika na maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.”

Malengo ya Maendeleo Endelevu yalipitishwa Septemba 25 na nchi zote 193 wanachama ya Umoja wa Mataifa katika mkutano maalum wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York. Malengo haya yataanza kutumika rasmi ifikapo Januari 2016.